DKT. MWINYI: MASHINDANO YA QUR'AN YAMEIBUA VIPAJI, KUKUZA MAADILI


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa mashindano ya kuhifadhi Qur’an yamekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana pamoja na kukuza maadili mema katika jamii.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo  05 Aprili 2026, katika dhifa ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Jumuiya ya Tuzo za Kimataifa za Kuhifadhi Qur’an Tukufu, iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.

_Rais Alhaj Dkt. Mwinyi akijadiliana jambo na Sheikh Badr bin Muhammad Al-Turki wa Msikiti wa Al-Haram, Makkah, wakati wa hafla hiyo._

Ameeleza kuwa mashindano ya kuhifadhi Qur’an siyo tu mashindano ya Kitabu Kitukufu, bali pia ni kielelezo cha kuitambulisha Tanzania yenye amani duniani kote.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wageni na washiriki wa mashindano ya kuhifadhi Qur’an kuwa Tanzania iko salama, yenye umoja na mshikamano unaojidhihirisha kupitia mkusanyiko huo, na kuwashukuru pamoja na kuwakaribisha nchini.

Rais, Alhaj Dkt. Mwinyi, akijumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ishaa iliyoongozwa na Sheikh Badr bin Muhammad Al-Turki.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwasihi waumini wa dini ya Kiislamu kushikamana na mafundisho ya Qur’an na Sunna za Mtume (SAW), na kuhimizana umuhimu wa kuzingatia maadili mema, kuwasimamia vijana katika mienendo yao sambamba na kulipa umuhimu mkubwa suala la kudumisha amani.

Rais Dkt. Mwinyi ameisisitiza jamii kuendelea kuimarisha maadili mema na kupambana na mmomonyoko wa maadili kwa kutumia mwanga wa Qur’an Tukufu, kwa kuzingatia kuwa ni dira na muongozo wa wanadamu katika maisha ya duniani.

Rais, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akipokea tunzo maalum iliyotolewa na Jumuiya ya Tuzo za Kimataifa za Kuhifadhi Qur’an Tukufu, kutoka kwa Mufti na Sheikh Mkuu, Sheikh Mkuu Tanzania, Abubakar Zubeir Bin Ally, wakati wa hafla hiyo.

Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Tuzo za Kuhifadhi Qur’an Tanzania chini ya uongozi wa Sheikh Othman Ali Kaporo kwa kuendeleza mashindano hayo kwa mafanikio, pamoja na kuandaa dhifa hiyo ya chakula cha usiku kwa washiriki.

Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni mgeni maalum, Sheikh wa Msikiti wa Al-Haram wa Makkah, Sheikh Badr bin Muhammad Al-Turki, pamoja na Balozi wa Saudi Arabia nchini. Yahya Bin Ahmed Okeish.

Rais, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mashindano ya Qur’an kutoka mataifa mbalimbali, wakati hafla hiyo ya chakula cha usiku.

Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur’an yamefanyika tarehe Leo 5 Aprili 2026 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo mshiriki kutoka Libya, Ibrahim Hilal Zeydaan, amekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata pointi 99.12. Mshindi wa pili ni Saydina Al Ghalla kutoka Mauritania aliyepata pointi 99.06, na mshindi wa tatu ni Ahmed Karim Shehmadduf kutoka Urusi aliyepata pointi 98.75.

Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa tuzo mbili maalum za kutambua juhudi na mchango wake katika kuendeleza masuala ya dini ya Kiislamu nchini, zilizotolewa na Ubalozi wa Saudi Arabia na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA