DKT. KIJAJI: WENYE MAHOTELI JIANDAENI NA WATALII WA AFCON 2027
WAMILIKI wa Hoteli nchini wametakiwa kujipanga na kuboresha huduma zao ikiwemo miundombinu ya malazi na chakula kuelekea AFCON 2027, Tanzania ikikadiriwa kuapokea watalii laki tatu kwa siku.
Akizungumza 23 Aprili 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu ya malazi katika Hifadhi ya Pori Tengefu, Mto wa Mbu Wilayani Monduli, Mkoani Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema Tanzania inatarajiwa kupokea idadi kubwa ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi, na kuwataka wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni kujipanga ipasavyo ili kunufaika kikamilifu na fursa hiyo.
Dkt. Kijaji ambaye aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Nkoba Mabula pamoja na viongozi wengine wa wizara alisema kuwa mashindano ya AFCON 2027 yatatoa fursa kubwa ya kiuchumi kwa nchi, hivyo ni wajibu wa wadau wa sekta ya utalii, kuhakikisha wanatoa huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa.
“Ni muhimu kwa kila mmiliki wa hoteli kuhakikisha anajiandaa vyema ili kuwahudumia wageni kwa ubora unaostahili,” alisema Dkt. Kijaji.
Alibainisha kuwa ujio wa AFCON 2027 katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania ni fursa adhimu kwa wananchi kunufaika kiuchumi na kukuza sekta ya utalii.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kijaji alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ubora wa huduma ili kuendana na mahitaji ya soko la kimataifa.
Mashindano ya AFCON 2027 yanatarajiwa kufanyika katika nchi za Afrika Mashariki na Tanzania ni miongoni mwa wenyeji wa tukio hilo kubwa la michezo barani Afrika, linalotarajiwa kuvutia maelfu ya wageni kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.






Comments
Post a Comment