DKT. ABBAS: SERIKALI HAIJASIMAMISHA WALA KUZUIA UWINDAJI WA KITALI


                                           Na Anangisye Mwateba-Arusha 

SERIKALI imesema haina mpango wa kusimamisha ama kuzuia shughuli za uwindaji wa kitalii na badala yake inaendelea kuandaa na kuboresha sera, sheria na miongozo itakayohakikisha uwindaji wa kitalii unafanyika kwa kuzingatia uhifadhi wa wanyamapori, kukuza mapato ya Taifa na kuchochea maendeleo ya jamii.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi kati ya Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji Tanzania ( TAHOA), Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas alisema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuenzi sekta ya wanyamapori kwakuwa ni rasilimali ya kipekee yenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii na hivyo haina mpango wa kuisimamisha bali kuiendeleza.


 _Mwenyekiti wa TAHOA, Michel Mantheakis, akizungumza wakati wa mkutano huo._

Ameongeza kuwa ni matarajio ya mkutano huo kuwa utabainisha mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uwindaji wa kitalii ili kujenga ustawi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la uwindaji wa kitalii Kimataifa.

Amewataka wadau hao wa uwindaji wa kitalii kuilinda sekta hiyo kwa kuzingatia maadili na kuendeleza uhifadhi na kupambana na ujangiri kutokukwepa kodi, kulipa kodi na stahiki za jumuiya au wananchi zinazozunguka maeneo ya uwindaji.

_Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora akizungumza wakati wa mkutano huo._

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora amesema mikutano ya aina hii imekuwa na tija kwa Serikali na wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika kutafuta suluhu ya changamoto kubwa zinazoikabili. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAHOA, Michel Mantheakis, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa sekta hiyo na kuongeza kuwa chama hicho kitaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na taratibu kwa kuwa kushuka ama kusimama kwa uwindaji wa kitalii ni kukosekana ama kushusha mapato ya serikali lakini pia kudhorota kwa uhifadhi na hivyo kutokomea kwa uwindaji wa kitalii.

Comments