ZANZIBAR YASHUKURU UHUSIANO NA OMAN


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Oman kwa kuendelea kutoa misaada inayochangia maendeleo ya Zanzibar.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Machi 2026, katika futari iliyoandaliwa na Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Balozi Said Salim Al-Sinawiy, iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Oman imeendelea kuwa na uhusiano wa kidugu na Zanzibar, na kwamba misaada inayotolewa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, utalii, urithi wa Mji Mkongwe na utamaduni imekuwa nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya Zanzibar. 

Aidha, ameihakikishia Oman kuwa Zanzibar itaendelea kudumisha ushirikiano wa karibu.

Rais Dkt. Mwinyi amewaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi na dunia ili kuepusha majanga mbalimbali pamoja na mifarakano miongoni mwa mataifa.


Vilevile amemshukuru Balozi wa Oman kwa kuendeleza utaratibu wa kuandaa futari hiyo kila Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hatua ambayo imekuwa ikiwaunganisha watu na kuimarisha umoja na upendo.

Kwa upande wake, Balozi Said Salim Al-Sinawiy amemhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa Oman itaendelea kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya Zanzibar. Pia amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake unaoleta maendeleo makubwa na kuahidi kuendelea kutoa msaada katika sekta za utalii, elimu, uchumi wa buluu, urithi wa Mji Mkongwe na utamaduni.

 



Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA