ZANZIBAR KUJITOSHELEZA UMEME, GESI, MAFUTA


                                         Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Andrew Lentz, kuzungumzia maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Marekani.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, tarehe 23 Machi 2026, Ikulu, Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amemueleza Kaimu Balozi Lentz kuwa Zanzibar ina mipango na mikakati madhubuti ya kuhakikisha inajitegemea na kujitosheleza katika masuala ya nishati ya mafuta na umeme, pamoja na kuwa kituo kikuu cha usafirishaji kupitia bandari kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.


Dkt. Mwinyi aamesema ujenzi unaoendelea wa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani unatarajiwa kumaliza changamoto hizo, na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar itaongezeka kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika, ikiwemo mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 200, matangi ya hifadhi ya mafuta, na bandari yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa, itakayosaidia kuondoa msongamano uliopo katika Bandari ya Malindi.

Amefahamisha kuwa ukuaji wa sekta ya uwekezaji nchini na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo umeifanya Zanzibar kutafuta njia mbadala za kujitegemea katika nishati ya umeme, mafuta na gesi, pamoja na kuleta mageuzi katika ujenzi wa Bandari ya Mangapwani.

Dkt. Mwinyi ameihakikishia Marekani kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kuishukuru kwa misaada yake kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, akibainisha kuwa bado zipo fursa nyingi kwa makampuni na wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza nchini

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Andrew Lentz, ameeleza kufurahishwa na hatua ya maendeleo inayofikiwa Zanzibar, hususan katika ujenzi wa miundombinu, akieleza kuwa ni kipaumbele muhimu kwa nchi inayolenga kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi pamoja na ustawi wa wananchi. 

Pia, ameahidi kuendelea kupanua maeneo ya ushirikiano na Zanzibar, hususan katika sekta za afya, mabadiliko ya tabianchi, biashara na uwekezaji.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA