VYUO VYA UDEREVA ZANZIBAR VYAPEWA MUDA KUJIBORESHA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukukuzi, Badriya Atai Masoud, ameviagiza vyuo vya Mafunzo ya Udereva Zanzibar kuchukua hatua za haraka kurekebisha kasoro zilizoainishwa, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika vyuo hivyo mbalimbali vya udereva akiwa na mamlaka za usalama barabarani.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo ya kusikiliza changamoto zinazovikabili vyuo hivyo na kutafuta njia ya bora ya kufuata, Naibu Waziri Badriya alisema wamegundua mapungufu kadhaa katika baadhi ya vyuo.
"Tumegundua mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa muhimu vya kufundishia" alisema na kuvitaja kuwa ni pamoja na mashine ya kupoza injini ya gari (Radiator), mfumo wa breki, Injini, mfumo wa mneso kwenye gari (Shockabsover), Mfumo wa mtengamano wa gari (Stabilizer) pamoja na ukosefu wa michoro sahihi kwenye viwanja vya mazoezi ya udereva.
"Tumebaini baadhi ya viwanja vya kujifunzia havikidhi vigezo na mahitaji kwa ajili ya kutoa mafunzo bora ya udereva" alisema Naibu Waziri Badriya ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kijini.
Alisema wamewataka wamiliki wa vyuo hivyo kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo na kushindwa kufanya hivyo kutailazimu serikali kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kusimamisha shughuli za vyuo husika au kufuta usajili wake.
Alibainisha kuwa lengo ni kuweka mikakati madhubuti itakayo saidia kupunguza ajali na kuimarisha usalama barabarani kwa manufaa ya wananchi wote.
Wamiliki wa vyuo hivyo licha ya kuishukuru serikali kwa ushirikiano wameomba kuongezwa kwa wasimamizi wa mitihani ya vitendo (kwa silva) ili kurahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma hiyo kwa wanafunzi wa udereva.






Comments
Post a Comment