RAIS DKT. SAMIA MGENI RASMI HARAMBEE UPANDIKIZAJI FIGO, ULOTO
Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa imepanga kufanya harambee kwa ajili ya kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Selimundu (sickle cell) na kusaidia matibabu ya upandikizaji Figo kwa wananchi wenye uhitaji,katika kuelekea maadhimisho ya kutimiza miaka 10 ya hospitali hiyo.
Kauli hiyo imetolewa 31 Machi 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Prof. Abel Makubi,wakati akiongea na wanahabari na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka kumi ya Hospitali hiyo na kilele chake kimepangwa kufanyike 8 Mei 2026.
"Jambo hili tunalifanya Sisi Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), matibabu ya upandikizaji Figo na Uloto yanahitaji gharama kubwa sana, hivyo ni vigumu kwa Mtanzania wa kipato cha chini kumudu gharama hizo," amesema Prof. Makubi
Amesema, Mgeni Rasmi katika harambee hiyo anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Zanzibar harambee inatarajiwa kufanyika 11 Aprili 2026 na jumla ya TSh. Billion 7 zinatarajiwa kukusanywa.
Aidha, Prof. Makubi amesema hadi sasa, idadi ya watoto 28 wamepatiwa huduma hiyo,Watanzania wakiwa 27 na mtoto mmoja (1) kutoka nchi ya Congo DRC kwa gharama ya shilingi TSh.Bilioni 1.9, ambapo jumla ya TSh.Bilioni 1.3 zimeokolewa kama matibabu haya yangefanyika nje ya nchi.
"Hospitali kwa sasa ina hudumia wananchi kama Mil. 10 hivi,Na Kwa sasa Hospitali ina Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi zaidi ya 100 na inatoa huduma 20 za Ubingwa na 18 za Ubingwa Bobezi," amesema Prof. Makubi
Prof. Makubi ametoa wito kwa Mashirika, Taasisi, Makampuni,wadau mbalimbali pamoja na Wananchi kushiriki katika kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto na upandikizaji Figo kwa wananchi wenye uhitaji kwa kuchangia fedha kupitia Control Namba 995220798235 Kwa Jina: 'BMH Organ Transplant au Account" Namba 102501000407 (BOT) Jina: BMH Organ Transplant.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt. David Mwenesano aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Mfuko huo amesema, mfuko huo unatambua kuwa, huduma za matibabu ya upandikizaji Figo na Uloto ni ya gharama kubwa hasa ukizingatia kuwa matibabu haya hayapo kwenye vifurushi vya BIMA ya Afya (NHIF).
"Bado vifurushi vya NHIF, havijaanza kugharamia matibabu ya kupandikiza Uloto na Figo badala yake , Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kusaidia Watanzania wasio na uwezo na wenye kuhitaji huduma hii muhimu," amesema Dkt. Mwenesano




Comments
Post a Comment