RAIS DKT. MWINYI, NYUMBA ZA WAHUDUMU AFYA, MASHINE YA MRI PEMBA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAKATI Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatimiza siku 100 madarakani, mashine ya Upigajipicha kwa Mwangi wa Sumaku (MRI) katika Hospitali ya Abdallah Mzee, wilaya ya Mkoani Kusini Pemba na nyumba za wahudumu wa afya katika hospitali za wilaya, vinatajwa kuleta mageuzi makubwa sekta ya afya, ambayo wananchi wanadai hawajawahi, wala kuyafikiria katika maisha yao.
Rais Dkt. Mwinyi katika sekta hiyo licha ya kufanya mambo makubwa miaka mitano iliyopita lakini bado anaendelea kusogeza huduma hizo jirani na wananchi.
Rais huyo ambaye anatekeleza na kuisimamia sera ya huduma za matibabu bila malipo kwa kila mZanzibari, amevunja na kujenga upya vituo vya afya na kuboresha huduma ili kulinda afya za wananchi wote, Unguja na Pemba.
Ujenzi huo wa miundombinu ya afya pia umezingatia makazi ya wahudumu wa afya kwani kila Hospitali ya wilaya kuna nyumba za madaktari na wahudumu wengine wa afya.
“Katika upande wa sekta ya afya katika siku 100, zipo alama Rais Dkt. Mwinyi kaendelea kuziweka kwa ajili ya maendeleo ya wananchi” anasema, Khamis Bilali Ali, Ofisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba.
Anasema kati ya mambo ya msingi ambayo zaidi ya miaka sitini hayajawahi kuwepo Pemba ikiwemo miradi ya kimkakati iliyozinduliwa rasmi ndani ya siku hizo lakini kubwa ni mashine ya MRI katika Hospitali ya Abdallah Mzee, Mkoani Kusini Pemba.
Mashine hiyo ambayo ina sumaku yenye nguvu kutengeneza picha za sehemu za ndani za mwili na ina uwezo mkubwa na matokeo sahihi zaidi ya T-Scan na mashine hiyo ndio imenza kazi ndani ya siku 100 za Rais Dkt. Mwinyi madarakani na kuleta matumaini mapya kwa wananchi wa Pemba.
“Hii huduma MRI, tulikuwa tukiihitaji kwa muda mrefu lakini ilitulazimu kusafiri hadi Unguja au Dar es Salaam lakini kutokana na maendeleo yaliyopo hivi sasa huduma inapatikana kwa wakati” anasema Salama Ali Khamis, Mkazi wa Kipangani, Wete Pemba.
Mashine hiyo na huduma zingine zilizoboreshwa katika hospitali hiyo, zinafungua tabasamu kwa wananchi wa visiwa hivyo.
“Tunampongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kutupatia huduma hii hapa, saa hii itakuwa huduma ya daladala kuja Hospitali kupata huduma. Huduma hii ipo na ni bure’ anasema Harduu Hamad Rashid, Mkazi wa Uweleni, Pemba.
Daktari Dhamana wa Hospitali ya Abdallah Mzee Pemba, Aboud Khamis Maabad anasema mashine hiyo ni ya kisasa na yenye uwezo mkubwa na hadi sasa imeisha wahudumia wagonjwa zaidi ya thelasini na awali haikuwepo lakini ndani ya siku hizo wameipokea na imeanza kutoa huduma.
“Kuja kwa huduma kumewapunguzia gharama kubwa walizokuwa wakipata ukizingatia hali za maisha za wananchi walio wengi” anasema Dkt. Dkt. Aboud Maabadi.
Uwepo wa makazi ya wahudumu wa afya katika hospitali zote za wilaya, Unguja na Pemba limekuwa ni jambo lenye msaada mkubwa kwa wagonjwa.
“Uwepo wa nyumba karibu kumerahisha hata inapotokea dharula inakuwa rahisi kuliko kutokea mbali na hapa” anasema Eli Mwasenga, Mhudumu wa Afya, Mwera Pongwe.
“Leo huduma na kila kitu kinapatikana, juzi nimemleta mzazi, dakika mbili kafanyiwa operesheni, naambiwa mzazi huyo hapo, juu ya kitanda na watoto wake wawili pacha” anasema Maua Khamis Sateni, Mkazi wa Vitongoji, Pemba.
Ahadi za Pemba zimetimizwa Unguja pia na Rais Dkt. Mwinyi mara kadhaa amekuwa akimtanguliza Mwenyezi Mungu na kusema yote waliyoahidi kwa uwezo wake yanafanyika, tena kwa wakati, akihimiza kudumishwa amani na utulivu uliopo ili mambo makubwa zaidi yaweze kufanyika.


Comments
Post a Comment