RAIS DKT. MWINYI AWASISITIZIA VIONGOZI WAKUU TAASISI ZA UMMA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza viongozi wakuu katika taasisi za umma kuzingatia upendo, uadilifu na haki katika kuwasimamia wanaowaongoza pamoja na utekelezaji wa majukumu yao.Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa viongozi wa umma kulitumia Kongamano la Tatu la Kiimani kwa Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama dira ya kuimarisha maadili katika utumishi wa umma na kusimamia majukumu yao kwa wema, uadilifu, haki na busara, wakitambua kuwa uongozi ni dhamana.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekemea suala la upendeleo katika taasisi za umma na kuwasisitiza viongozi kuwa mfano mwema kwa wanaowaongoza, kuonesha upendo pamoja na kuwa tayari kupokea ushauri kutoka kwao.
Amebainisha kuwa taasisi zinazofanya vizuri katika utumishi wa umma ni zile zinazoongozwa kwa upendo, haki, uadilifu na uwajibikaji, mambo yanayochangia ufanisi katika utendaji wa Serikali.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza viongozi kuyazingatia maelekezo yaliyotolewa na Masheikh katika mada mbalimbali za kongamano hilo, na kuyatumia kama nyenzo ya kuimarisha utendaji wao kwa kuzingatia misingi ya kiimani.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameipongeza Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kwa kuandaa kwa mafanikio kongamano hilo kwa miaka mitatu mfululizo.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini pamoja na watumishi wa SMZ.







Comments
Post a Comment