MBETO: WEKEZENI ELIMU YA DINI KWA WATOTO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Saalam
WAISLAM nchini wametakiwa kuwekeza kwenye elimu ya dini kwa watoto wao ili wawe wema wenye kumjua Mungu hali ambayo itawafanya wafanye vizuri hata katika tahsusi zingine.
Akizungumza 29 Februari 2026 katika Shindano la 3 la Usomaji Quraan lililoandaliwa na Taasisi ya I'MAADUD-DIN Foundition na kufanyika Yombo Vituka, Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema hakuna bidhaa njema kama mtoto mwema.
Alisema mtoto hata akisomeshwa na kuwa na PHD kama hana hofu ya Mungu, hamna kitu na atakuwa hana msaada kwa wazazi wake Duniani na hata kesho akhera.
"Niwape siri msishtuke hao mnaoambiwa maprofesa, wengine wana PHD, wachunguzeni, wana hofu ya Mungu? Wasiokuwa nayo hamna kitu, wataiba, wataongeza maziro (sifuri), atapiga, ataona duniani kapata" alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa matokeo yake akifariki hazikwi na chochote ataacha watu wanagombania mali zake.
Mbeto ambaye aliwahimiza waumini hao kusoma Quraan aliwataka waumini kuichangia dini yao na kuwawezesha walimu wa madrasa ambao wanajukumu kubwa la kufundisha dini ya kiislamu na kuwahimiza kuwa wanapofuatwa kwa uwezeshaji wafanye hivyo ili uislam uzidi kusonga mbele.
Katika shindano hilo ambalo kauli mbiu yake 'Quraan ni Amani tuilinde', Mbeto alisisitiza kuwa Islam maana yake amani.
"Naomba niwasisitizie tuitunze amani yetu kwani bila amani hakuna ambalo linaweza kufanyika" alisema Mwenezi Mbeto.

Comments
Post a Comment