MBETO: MAGUFULI ALIKUWA SHUJAA MZALENDO WA TAIFA

                                            Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati John Pombe Magufuli alikuwa shujaa mzalendo aliyepigania maslahi mapana ya nchi ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Bahari FM leo 17 Machi 2026, kuhusiana na miaka mitatu toka kifo cha Rais huyo wa awamu ya tano, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis alisema alikuwa na mapenzi makubwa kwa nchi na chama chake CCM.

Mbeto alisema kati ya mambo aliyofanya ni pamoja na miradi ya kimkakati ya Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Reli ya treni ya umeme, aliimarisha usafiri wa anga, miundombinu ya barabara, ujenzi wa daraja la Kigongo/Busisi, Tanzanite, mwendokasi, ununuzi wa ndege mpya na mengine.

"Miongoni mwa mambo ambayo waTanzania hatutasahau ni kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma" alisema mwenezi Mbeto na kuongeza kuwa hilo lilikuwa wazo la toka enzi za Mwalimu (Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) ambalo lilishindwa kutekelezeka.

"Yeye ndio aliamua na sasa hivi yamekuwa makao makuu ya nchi na serikali. Dodoma inazidi kujengwa, imebadilika" alisema na kuongeza kuwa ni maamuzi ya ujasiri aliyoamua kuchukua.

Alibainisha kuwa  chini yake nchi ikaingia uchumi wa kati na mathalani alijua ni ngumu kushawishi uwekezaji wakati hakuna uhakika wa nishati ya umeme ndio maana lilijengwa Bwawa hilo la kuzalisha umeme ambao unaweza kuuzwa pia katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko.

Mwenezi huyo alisema, hayati Magufuli alikuwa na ujasiri mkubwa katika kutetea raslimali za nchi na hakusita kumtaja mbadhirifu yeyote na hata kumtumbua hadharani na alisimama kidete kuhakikisha raslimali za nchi haziporwi kiholela akitoa mfano wa uamuzi wa kupiga marufuku usafirishaji mchanga kwenda nje kuchenjua dhahabu.

"Pia alihakikisha makampuni yote ya madini yanalipa kodi stahiki na pia nidhamu ya kazi kwa watendaji serikalini na hakujali undugu, urafiki, mtoto wa ndugu, mjomba na aliangalia uwezo na utendaji kwa maslahi mapana ya nchi" alisema.

Mbeto anataja upanuzi wa bandari za Tanga, Mtwara, Da es Salaam na viwanja vya ndege na kuweka mifumo mizuri ya kodi na pia alizisimamia mali za chama na maslahi ya wanachama na viongozi.

"CCM ni chama kikubwa nchini, kina raslimali nyingi lakini zilinufaisha wachache na alitaka kuhakikisha viongozi wa chama wanalipwa vizuri kama waliopo serikalini" alisema Mbeto.

Alibainisha mwenezi huyo kuwa alifanikiwa na alianza kuboresha maslahi ya watumishi wa CCM na mambo mengine mengi ambayo yanafanya wanaCCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kumkumbuka.

"Tutamkumbuka kwa ujasiri na uzalendo wa kupigania maslahi mapana ya nchi yetu" alisema Komredi Mbeto na kutaka aenziwe kwa watendaji kuchukia rushwa na mambo yote ya hovyo yanayoligharimu Taifa.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA