DKT. MWINYI: MASHINDANO QUR'AAN ZANZIBAR KITAMBULISHO KNGINE KIMATAIFA


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema mashindano ya Dunia ya Kuhifadhi Qur’aan yamekuwa kivutio na kitambulisho chengine cha Zanzibar Kimataifa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Machi 2026, katika Mashindano ya Tatu ya Dunia ya Kuhifadhi Qur’aan yaliyofanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.


Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wafadhili na wadau mbalimbali kuendelea kuyaunga mkono mashindano hayo ili nchi iendelee kunufaika na faida mbalimbali zinazotokana na kufanyika kwake.

Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kushika muongozo wa Qur’aan ili kuwa na jamii iliyoongoka, pamoja na kushikamana na Sunna za Mtume Muhammad ili kuongozwa na kupata fadhila za Mwenyezi Mungu.


Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza washiriki na washindi wa mashindano hayo kujifunza tabia njema, akieleza kuwa lengo si kupata cheti pekee bali ni kuishi kwa nidhamu na kukuza utamaduni wa Kiislamu katika maisha yao ya kila siku.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na Shirika la Utangazaji Zanzibar  (ZBC) kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo kwa mafanikio kwa miaka mitatu mfululizo.

Aidha, amewapongeza wafadhili na wadau mbalimbali kwa michango waliyoitoa kufanikisha mashindano hayo makubwa.

Pia amewapongeza washiriki wote kwa kazi kubwa na nzuri waliyoionesha katika mashindano hayo, jambo linalodhihirisha kazi njema inayofanywa na wanazuoni na walimu wa Qur’aan.

Mashindano ya mwaka huu ya Kuhifadhi Qur’aan yameshirikisha washiriki kumi na mmoja (11) kutoka mataifa mbalimbali, na mshiriki kutoka Zanzibar, Abdulaaziz Ali Khamis, amekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata pointi 99.5 na kuzawadiwa shilingi milioni 30. Mshindi wa pili ni Ibrahim Usman Ibrahim kutoka Nigeria aliyepata pointi 99 na kuzawadiwa shilingi milioni 20, huku mshindi wa tatu akiwa Adan Ismail kutoka Marekani aliyepata pointi 98.5 na kuzawadiwa shilingi milioni 10.

Mashindano hayo yalihusisha vipengele vya kuhifadhi Juzuu 30 za Qur’aan, usomaji wa Adhana pamoja na kipengele cha usomaji wa Qur’aan kwa mtindo wa Tashjih Tahakik.



Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA