DKT. MWINYI: BANDARI MANGAPWANI KUKUZA UCHUMI ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kukamilika kwa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kutokana na fursa za kiuchumi zitakazojitokeza.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 22 Machi 2026, akiwa katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dkt. Mwinyi amezitaja changamoto tatu ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar kwa sasa, kuwa ni pamoja na ukongwe na uchakavu wa Bandari ya Malindi, hali inayosababisha kushindwa kuhudumia meli kwa haraka na hivyo kuchukua muda mrefu kusubiri kushusha mizigo.

Changamoto ya pili ameitaja kuwa ni uhaba wa umeme wa kutosha, pamoja na ukosefu wa hifadhi ya mafuta ya kutosha, hali inayosababisha gharama za nishati kupanda.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imejiandaa kuyaondoa matatizo hayo kwa pamoja baada ya kukamilika kwa mradi huo wa kimkakati wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, utakaokuwa na uwezo wa kuhudumia meli aina ya Ultra Large Container Vessel zenye uwezo wa kubeba hadi makontena 15,000 kwa wakati mmoja, pamoja na kuhudumia zaidi ya makontena 200,000 kwa mwaka.

Ameeleza kuwa Zanzibar itakuwa kitovu cha huduma za usafirishaji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Ameeleza kuwa bandari hiyo pia itakuwa na eneo la matangi ya kuhifadhia mafuta na zaidi ya lita milioni sita zitahifadhiwa, hatua itakayochangia kushusha gharama za mafuta nchini.

Aidha, kutakuwepo na mtambo wa kuzalisha umeme wenye uwezo wa kuzalisha megawati 200.

Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kufanikiwa kwa hatua hizo kutachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Pia amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa katika kufanikisha mradi huo, na kuwahakikishia wale wote waliopisha mradi huo kuwa watapata stahiki zao bila ya kudhulumiwa.

Mapema, Mwenyekiti wa Kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited, Bw. Bai Yinzhan, amesema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha inatekeleza ujenzi huo kwa wakati huku ikizingatia viwango vya kimataifa, na kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya kiuchumi Zanzibar.

Aidha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Muhammed, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali, na kueleza kuwa mradi huo utakuwa mkombozi na chanzo kikubwa cha fursa za ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Zanzibar kwa ujumla.

Akiwasilisha taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Ali Said Bakari, amesema ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 300, na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2028, ukiwa na uwezo wa kuhudumia makontena zaidi ya tani milioni moja za mizigo kwa mwaka.

Uwekaji huo wa jiwe la msingi ulienda sambamba na makabidhiano ya vitalu vya ujenzi wa hifadhi ya kimkakati ya mafuta na gesi, vitakavyotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya One Petroleum na Shirika la Bandari la Zanzibar, pamoja na makabidhiano ya vitalu vya ujenzi wa bohari za mafuta kwa kampuni za Puma, Gapco na Zanzibar Petroleum (ZP), zitakazohamisha miundombinu yake na kujenga bohari mpya Mangapwani.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA