DKT. MWINYI ATAKA USHIRIKIANO KISEKTA MKUMBI-II
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano madhubuti kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI-II), ili kufikiwa kwa haraka malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo 27 Machi 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, katika Mkutano wa Uhakiki wa Rasimu ya MKUMBI-II, ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta za umma na binafsi.
Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kipato cha juu ifikapo mwaka 2050, ikiwa ni pamoja na kufikia uchumi wa thamani ya Dola za Marekani trilioni 1 na kuongeza kipato cha mtu binafsi angalua Dola 7,000 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa kufanikisha azma hiyo kunahitaji ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka, jambo linalohitaji uwekezaji mkubwa katika sekta za uzalishaji.
Amefafanua kuwa mafanikio ya dira hiyo yanategemea kwa kiwango kikubwa mchango wa Sekta Binafsi, hususan kupitia uwekezaji katika viwanda, kilimo cha kisasa, uchumi wa buluu na huduma zenye thamani kubwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wenye tija na ushindani wa kimataifa pamoja na kuendelea kuunda ajira kwa wananchi, hususan vijana.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeanza kuona matokeo chanya ya jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na mwaka 2024 miradi ya uwekezaji 901 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 9.3 ilisajiliwa na kutarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 212,000.
Katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025, jumla ya miradi 1,828 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 20.3 ilisajiliwa nchini.
Katika kuimarisha mazingira hayo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya mapitio ya sheria zaidi ya 94 ili kuondoa vikwazo vya biashara au kupunguza zaidi tozo na kodi 628 zilizokuwa kikwazo, pamoja na kuunganisha mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Serikali pia imeendelea kuimarisha miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli, bandari, barabara, nishati na TEHAMA ili kuwezesha ukuaji wa uchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar nayo imeendelea kunufaika na maboresho hayo kupitia ukuaji wa sekta za utalii, uchumi wa buluu na huduma za kifedha, hali inayochangiwa na mazingira bora ya uwekezaji yanayoimarika.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na Washirika wa Maendeleo wakiwemo Umoja wa Ulaya (EU) ambao wamechangia utekelezaji wa MKUMBI ya awali na maandalizi ya MKUMBI-II.
Kuhusu maandalizi ya MKUMBI-II, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa mchakato wake umezingatia ushirikishwaji mpana wa wadau wa sekta binafsi na umma kwa lengo la kuhakikisha mpango huo unajibu changamoto halisi za uwekezaji na biashara nchini.
Amefafanua kuwa rasimu iliyowasilishwa imejikita katika kuboresha utoaji wa huduma kwa haraka na kwa ufanisi, kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, kuweka mazingira rafiki yenye uwazi na yanayotabirika kwa wawekezaji, pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa mafanikio ya MKUMBI-II yatategemea kwa kiasi kikubwa uwajibikaji wa pamoja na ushirikiano endelevu kati ya Serikali na Sekta Binafsi, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuboresha huduma na kuongeza tija.
Akihitimisha hotuba yake Rais Dkt. Mwinyi amehimiza washiriki wa warsha hiyo kutumia kikamilifu fursa ya uhakiki wa rasimu kwa kutoa maoni, uzoefu na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mpango huo kabla ya utekelezaji wake rasmi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji (SMZ), Sharif Ali Sharif, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaendelea kuchukua hatua mbalimbali madhubuti za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, jambo ambalo ni hitaji la kimkakati katika dunia ya leo yenye ushindani mkubwa wa kiuchumi.
Ameeleza kuwa mageuzi hayo yanalenga kujenga uchumi jumuishi unaoshirikisha kikamilifu sekta binafsi kama injini kuu ya ukuaji wa uchumi, na kupitia mazingira wezeshi nchi itaweza kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, kuongeza uzalishaji, kupanua ajira na kuimarisha maisha ya wananchi.
Upande mwingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (JMT), Profesa Kitila Mkumbo, amesema kuwa rasimu ya MKUMBI-II imebainisha changamoto 59 ambazo zinakwamisha ufanyaji wa biashara nchini ikiwemo Zanzibar.
Ameeleza kuwa kwa kuzingatia changamoto hizo, rasimu hiyo imependekeza maeneo 11 ya kufanyiwa kazi pamoja na kubainisha hatua 246 za kuchukuliwa kwa lengo la kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Naibu Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wa taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara, wawekezaji, viongozi wa dini, wanahabari pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.





Comments
Post a Comment