WAZIRI KAIRUKI ATAJA MAMBO MATATU SEKTA MAWASILIANO
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Sayansi na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki ametaka utendaji wenye weledi, maadili na ubora wa huduma katika kudumisha misingi na maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kikao kazi baina ya wizara, bodi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma 27 Februari 2026 aliiwataka menejimenti na bodi kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji, weledi, uwazi na uadilifu katika utendaji wa kazi ili wananchi wapate huduma bora na zenye tija.
Waziri Kairuki ametaka misingi imara ya maendeleo inajengwa, uongozi thabiti na usimamizi bora wa raslimali za umma.
Pia amewataka watendaji hao kuongeza kasi ya uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu hususan kwenye maeneo yasiyo na huduma muhimu ili kuinua wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano ili kupunguza pengo kati ya mijini na vijijini.
Waziri Kairuki ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, amesisitiza kampeni za elimu kwa umma na vyombo vya habari, mitandao ya habari na mikutano ya hadhara ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo pia kujilinda dhidi ya changamoto za kidijitali.
"Muhimu kukuza na kutumia wataalam wazawa kuwezesha mafunzo na kuongeza wa watumishi ili kuendana na mabaadiliko ya teknolojia na kuhakikisha uendelevu wa miradi ya kimkakati" alisema.
Waziri huyo amesisitiza, ushirikiano, kufanyakazi pamoja na ubunifu na uwajibikaji wa hali ya juu na utekelezaji madhubuti wa maelekezo hayo utaimarisha huduma, kuongeza imani ya wananchii na kuchochea kasi ya maendeleo ya sekta ya mawasiliano na Taifa kwa ujumla.




Comments
Post a Comment