WATENDAJI SMZ WATAKIWA KUFUATILIA MWENENDO BEI ZA VYAKULA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WATENDAJI wenye dhamana katika sekta ya biashara katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wametakiwa kufuatilia mwenendo wa bei za vyakula katika masoko Unguja na Pemba ili kuwalinda wananchi dhidi ya mfumuko wa bei usio wa lazima.
Akizungumza Ofisini kwake Mjini Unguja 23 Februari 2026, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo Khàmis Mbeto Khamis alisema kuna bidhaa za vyakula ambavyo serikali ilitoa bei elekezi kabla ya kuanza mfungo wa Ramadhani.
Mbeto ambaye karibuni alifanya ziara katika masoko ya Unguja, alisema baadhi ya bidhaa kama unga wa ngano, mafuta ya kula na zingine bei elekezi ilitolewa hivyo wana wajibu wa kuhakikisha bei hizo rafiki kwa wananchi zinafuatwa.
Pia Mwenezi Mbeto amewataka wafanyabiashara kuzingatia maadili na kutopandisha bei za vyakula kwa lengo la kutengeneza faida zaidi kwani kufanya hivyo ni kuwaumiza wananchi hususan wale wenye kipato cha chini.
"Kuongeza bei za vyakula kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan ni kuwaumiza wananchi hususan wale wanyonge na si kitendo cha utu na ubinadamu" alisema na kuwataka kufuata bei elekezi kwa baadhi ya bidhaa na zingine kutopandisha bei kwa misingi ya kuvuna faida zaidi.

Comments
Post a Comment