WAISLAM WAKUMBUSHWA IBADA, MATENDO YA HURUMA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa kuisoma, kuihifadhi na kuzingatia mafundisho ya Qurani Tukufu miongoni mwa vijana ili kujenga kizazi chenye maadili, hofu ya Mwenyezi Mungu na mchango chanya katika jamii.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 22 Februari 2026, katika Mashindano ya Kitaifa ya Qurani Tukufu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aisha Sururu Foundation, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, na mashindano hayo yamewakutanisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, yakidhihirisha mshikamano wa kiTaifa na kukuza vipaji vya usomaji wa Qurani nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Taasisi ya Aisha Sururu Foundation kwa kuendeleza utaratibu wa kila mwaka wa kuandaa mashindano hayo, akibainisha kuwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha mapenzi ya Qurani kwa vijana na kuwajengea msingi imara wa kiimani.
Amelishukuru pia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mashindano hayo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza walimu, Masheikh na majaji kwa juhudi zao katika kuwaandaa washiriki na kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa uadilifu na weledi.
Alisema, juhudi hizo ni uwekezaji wa moja kwa moja katika kujenga jamii yenye maadili na mshikamano.
Rais Dkt. Mwinyi ambaye aliambatana na mkewe Maria m Mwinyi, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini kuongeza juhudi katika ibada ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na kuimarisha matendo ya huruma na ukarimu kwa kuwasaidia watu wenye uwezo mdogo, wajane na mayatima, akieleza kuwa hatua hiyo huleta baraka, kuimarisha mapenzi na kuendeleza amani katika jamii.
Mashindano hayo yamejumuisha kuhifadhi Qurani Tukufu kuanzia Juzuu 3, 5,10, 20 na Juzuu 30 kwa washiriki wa kike na wa kiume, pamoja na makundi maalum, ambapo Said Rashid Bakari kutoka Dar es Salaam ameibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha kuhifadhi Juzuu 30 na kutunukiwa zawadi ya shilingi milioni 5.
Mashindano hayo pia yaliambatana na utoaji wa Tuzo Maalum, ambapo kwa heshima na kumbukumbu ya Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Dkt. Mwinyi alipokea tuzo hiyo kwa niaba yake, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuenzi, kuhamasisha na kuendeleza mafundisho ya Qurani Tukufu
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Mama Mariam Mwinyi, viongozi wa dini, wadhamini, washiriki wa mashindano pamoja na wananchi kwa ujumla.









Comments
Post a Comment