MTANZANIA AWEKEZA TSH.BILIONI 8 JIJINI MBEYA
Na Mwandìshi Wetu, Mbeya
Katika ziara ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani iliyofanyika leo tarehe 16 Februari 2026 jijini Mbeya, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetembelea mradi wa City Park Garden unaomilikiwa na BABITO Trading Company Limited.
Mradi huo uliopo katikati ya Jiji la Mbeya ni kituo cha kisasa cha burudani na starehe kilichogharimu shilingi bilioni 8 na kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 100. Uwekezaji huo umejengwa katika eneo la Bustani ya Jiji lenye ukubwa wa hekta 3.67 na umeongeza thamani ya kiuchumi na kijamii katika mkoa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Godlisten Msuya amesema mradi huo unajumuisha migahawa mitatu, kumbi tatu za mikutano na sherehe, mabwawa mawili ya kuogelea, vyumba 93 vya biashara, maegesho ya magari, maeneo ya michezo ya watoto pamoja na sehemu za kisasa za kuoshea magari. Ameeleza kuwa mafanikio ya uwekezaji huo yametokana na ushirikiano mkubwa na TISEZA, ambayo ilitoa vivutio mbalimbali ikiwemo punguzo la ushuru wa forodha kwa asilimia 75 kwenye mashine na vifaa vya uzalishaji vilivyoingizwa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji kutoka TISEZA, Bw. Daudi Riganda, ametoa wito kwa Watanzania kutumia fursa za vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na mamlaka hiyo, wakifuata mfano wa BABITO Trading Company Limited, ili kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani jijini Mbeya na Tanzania kwa ujumla kwa maendeleo endelevu ya Taifa.




Comments
Post a Comment