MKUTANO MAKATIBU WAKUU KUELEKEA WATAALA WA UKIMWI SADC


                        Na Shaban Juma, WAF-Johannesburg, Afrika Kusini

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Daud Tayari, ameongoza ujumbe wa wataalam kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki katika mkutano wa Makatibu Wakuu na wataalamu wa afya pamoja na masuala ya UKIMWI na VVU wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo umeanza leo 21 Februari 2026 jijini Johannesburg, ukiwa mahsusi kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Afya na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya UKIMWI na VVU wa SADC, unaotarajiwa kufanyika 24   Februari 2026.

Katika mkutano huo, nchi wanachama wa SADC zinatathmini kwa pamoja hali ya afya ya kikanda, dharura za afya ya jamii, pamoja na mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya katika nchi wanachama.

Maeneo mengine yanayojadiliwa ni pamoja na masuala ya lishe na uwasilishaji wa taarifa za magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI.

Vilevile, wajumbe wamejadili taarifa ya utekelezaji wa Huduma ya Ununuzi wa Pamoja wa SADC (SADC Pooled Procurement Services), inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa gharama nafuu, zenye ubora unaokubalika na zinazopatikana kwa wakati kwa nchi wanachama.

Mkutano huo pia umejadili taarifa kuhusu athari za mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katika baadhi ya nchi za ukanda wa SADC. Kufuatia hali hiyo, wajumbe wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za pamoja za kiKanda katika kukabiliana na dharura za afya ya jamii, hususan katika muktadha wa majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza.

Tanzania imezitaka nchi wanachama kuendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, mipango ya maandalizi na mikakati ya kukabiliana na majanga ili kupunguza athari kwa afya za wananchi.

Kwa upande mwingine, mkutano umeweka mkazo katika uimarishaji wa huduma za dharura na upasuaji, huduma za usingizi (anaesthesia) na uuguzi, hususan kwa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), afya ya uzazi na afya ya wanawake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuharakisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage) katika ukanda wa SADC.

                                 

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana na nchi wanachama wa SADC katika kuimarisha mifumo ya afya, kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuhakikisha wananchi wa ukanda huo wanapata huduma bora, salama na endelevu za afya.





Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA