MBETO: MABASI MAPYA YA UMEME SI MALI YA ZSSF


                               Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MABASI ya Umeme ambayo yamewasili Zanzibar wiki iliyopita na yanatarajiwa kuanza kutoa huduma wakati wowote kuanzia sasa ni ya wananchi na Mfuko wa Taifa wa Pensheni za Wafanyakazi Zanzibar (ZSSF) ni wakala anayefanyakazi na Serikali.

Akizungumza mara baada ya kurudi ziara ya kikazi nchini Spain katika Jiji la Madrid na Doha, Qatar alipokwenda kwa mwaliko maalum, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto Khamis alisema mabasi hayo ni ya wananchi hivyo wana wajibu wa kuyatunza.

Alisema pesa iliyotumika kununua mabasi hayo ni kodi za wananchi ambao ndio wenye mabasi yao na ole wake atakayejaribu kufanya uharibifu wa aina yoyote katika mabasi hayo.

Alibainisha kuwa mabasi hayo ya kisasa yana kamera za usalama hivyo aliwaonya wale watakaothubutu kufanya uharibifu wowote kuwa watakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.

“Yatakuwa na ulinzi wa kamera ndani ya mabasi hayo na mtu ukipanda na wembe wako ukakata kochi, hatukuachi tunataka tubadilike, ukifanya uharibifu wowote katika lile gari utakamatwa” alisema.

Alisema mabasi hayo yatafika hadi nje ya Mji kutokana na zaidi ya kilometa 109 za barabara za lami zilizozingatia watumiaji wote wa barabara wakiwemo waenda kwa miguu, zilizojengwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Alisema kukamilika kwa Flyover za Kwerekwe na Amani na barabara zake kutawezesha mabasi hayo kufika Fuoni, Jumbi na kwingineko.

“Fly Over ya Amani ikikamilika itawezesha mabasi hayo kuunganisha Mnazi Mmoja, Chukwani hadi Bungu ambako bara zake zimekamilika na zipo vizuri” alisema Mwenezi Mbeto.

Alisema Mwenezi huyo kuwa mabasi hayo mapya ni safari ya kuelekea Zanzibar mpya, tunayoitaka na kwamba maono ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni makubwa ambayo yanahitaji kupewa ushirikiano na awali kabla ya ziara hiyo alikuwa anashangaa kwanini nchini hatufanikiwi katika mambo mengi lakini alichokugundua ni kuwa watu wanatakiwa kuwajibika na kufuata sheria zilizopo.

Alisema wenzetu wamejenga miji yao pamoja na mambo mengine, wanazingatia usafi na utunzaji wa miundombinu yao.

Mbeto aliwatoa wasiwasi watoa huduma za usafiri (daladala), kuwa wanapaswa wajiongeze kwani maendeleo ni lazima na wanaweza kupeleka vyombo vyao katika ruti zingine.

“Huwezi kupata maendeleo kwa kuendelea kupanda gari mbavu za mbwa au Coaster, tukitaka maendeleo tukubali kubadilika na ndivyo maendeleo yalivyo hata huko kwenye Metro (Treni chini ya ardhi) na za juu watu walipoteza ajira” alisema.

Alibainisha kuwa ajira zipo na kinachotakiwa ni ubunifu na si lazima gari hizo kuja mjini na serikali haiwezi kuacha kufanya maendeleo kwa kuwa fulani ana gari zake zinafanyabiashara mjini.

“Tukiacha kufanya maendeleo kwa kuwa eti Mwenezi ana Coastar zake, Toyota Hiace au Chai Maharage yake hatuwezi kufika na kuna ambao wanasema ooh...., tutawezaje kubeba mizigo toka shamba, ni suala la muda na zitakuja gari kwa ajili ya mizigo tu ambazo hadhi yake itaendana na miundombinu iliyotengenezwa na Dkt. Mwinyi” alisema Mbeto.

Alisema suala la usafi katika miji ya Zanzibar bado changamoto kulinganisha na majiji mengine yakiwemo Doha Qatar na Madrid Spain na kuwataka wananchi kubadilika.

Siku ya mapokezi ya mabasi hayo 10 ya awali, ilielezwa kuwa madereva na watendaji wangine wa mabasi hayo watapewa mafunzo maalum kabla ya ajira.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA