MBETO: CCM IPO TAYARI KWA MAZUNGUMZO NA TAASISI, CHAMA CHOCHOTE


                                        Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kipo tayari kufanya mazungumzo na chama chochote cha siasa au taasisi yoyote lengo likiwa kujenga amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Katibu Katibu Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Cde: Khamis Mbeto Khamis, alisema hayo akirejea hatua ya hivi karibuni ya chama hicho kupokea taarifa ya maendeleo ya mazungumzo yanayotafuta Muafaka wa utatuzi wa Kisiasa yenye lengo la kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. 

CCM kimetaja mazungumzo hayo kuwa bado siri huku yakisimamiwa na Rais wastaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein. 

Taarifa ya uwepo wa mazungumzo baina ya CCM na ACT Wazalendo ilipokelewa na ilitangazwa kuridhiwa baada ya kukamilika kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa kilicho fanyika tarehe 19/2/2026 katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, 

Mbeto alisema Msingi wa mazungumzo hayo, umejiegemeza katika kuzipitia hitilafu, dosari na kasoro na changamoto mbalimbali za kisiasa na kisheria hatimae ziweze kurekebishwa.

Alisema pia katika majadiliano hayo zitaangaliwa kasoro na dosari kama zipo na endapo ni za kisheria, zitapelekwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

"Kamati Maalum ya NEC Zanzibar imepokea taarifa ya kuendelea kwa mazungumzo kati ya CCM na ACT na agenda za mjadala huo bado ni siri na hatma ya mazumgumzo hayo ikifikiwa zitatangazwa na pande zote mbili" alisema Mwenezi Mbeto.

"Katika Majadiliano ikiwa kutaonekana haja ya kubadili jambo husika kisheria, suala hilo litapelekwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kwa mfano huwezi kuondosha kura ya mapema bila kubadili sheria yake" alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema ni majadiliano yenye nia njema kwa mustakabali na ustawi wa Zanzibar na Wananchi wake.

"Wajumbe washiriki kwenye mazungumzo hayo watarudisha mrejesho kwa chama kilichowatuma kwa ajili ya hatua nyingine za vikao vya juu vya chama chetu zitafuata na kutoa maamuzi yake" alisema Mbeto.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA