MBETO: ACT 'INACHANGANYIKIWA'
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
UAMUZI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuteketeza karatasi zilizotumika katika uchaguzi Mkuu uliopita 29 Oktoba 2025 ni la kisheria na wanacholalamikia ACT Wazalendo ni kutafuta huruma za wapigakura wao na kupoteza muda wa kuwatumikia wananchi.
Akizungumza na Wanahabari Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, Zanzibar leo 06 Februari 2026, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 kifungu cha 98 (3) kinaipa mamlaka ZEC kuteketeza nyaraka zilizotumika kwenye uchaguzi uliopita ndani ya siku 90 labda kuwe na zuio la kuzuia utekelezaji wa nyaraka hizo.
"Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi, kasema kuwa hadi siku hizo zimekamilika hakukuwa na zuio lolote toka mahakamani sasa wao wanataka nini? " alihoji Mbeto.
Alibainisha kuwa ACT walipoenda mahakamani walidai ushahidi wanao na mahakamani unawasilisha madai yako na ushahidi sasa wao vipi wautake toka ZEC?
Alisema hiyo ni wazi kuwa wamechanganyikiwa na kupoteza mwelekeo kwa waZanzibari na waTanzania kwa ujumla.
Wiki hii ACT Wazalendo walitoa tamko la kulalamikia kitendo cha ZEC kuteketeza karatasi zilizotumika kupiga kura na kudai kuwa ni kupoteza ushahidi muhimu katika kesi walizofungua kupinga matokeo katika baadhi ya majimbo, Zanzibar.
"Pengine ni kutokujua sheria kwa sababu tume kama isingefanya hivyo katika muda uliowekwa ingekuwa imevunja sheria" alisema Mbeto na kuongeza kuwa ACT warudi kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza na kuzitumikia nafasi zao nne za Mawaziri na ile Makamu wa Kwanza wa Rais ambayo sijui watampa Othman Masoud au mtu mwingine, watajua wenyewe"" alisema Mbeto.
Mwenezi huyo alisema Ibara ya 15 ya Sheria ya Uchaguzi inaeleza utaratibu mzima wa upigaji kura kuwa kila kituo kitakuwa na wakala wa chama cha siasa waandikishaji ambaye atakuwa takwimu na data zote za wapiga kura.
Mbeto alisema Ibara 75 inazungumzia utaratibu wa kupiga kura, matokeo na utangazaji na kila kituo yupo wakala na karatasi ya matokeo anakuwa nayo.
"Kama sio kuchanganyikiwa ni nini? Kura zimepigwa, zimehesabiwa, mawakala walikuwepo kila mmoja na karatasi lake, uchaguzi umeisha wasubiri 2030" alisema hakuna njia ya mkato wafuate sheria na kurudi na kuunda serikali ili kuwatumikia wananchi wapigakura.
Alisema mwenezi huyo kuwa wasifikirie kuwa suala hilo linaweza kurudi kujadiliwa barazani na Rais Dkt. Hussein Mwinyi hawezi kubadili chochote bila kupitià vikao vya juu vya CCM ambavyo baadae vitoe maelekezo kwa serikali.
"Rai yangu kwao, waje tuwatumikie waZanzibari katika nafasi walizotuchagua, uchaguzi umeisha na hakuna njia ya mkato" alisema Mbeto.

Comments
Post a Comment