DKT. MWINYI : TUNAENDA KUTATUA CHANGAMOTO UCHUKUZI MIZIGO PEMBA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imejipanga vema kumaliza tatizo la usafiri na usafirishaji wa mizigo katika Kisiwa cha Pemba.
Alhaj. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 17 Februari 2026 alipoufungua Msikiti mpya wa Chachani uliopo Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, uliojengwa na mfanyabiashara Said Nassor Bopar.
Amefahamisha kuwa tayari Serikali imeandaa meli mbili za mwendo kasi kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa vyombo vya usafiri kwa wananchi wa Pemba. Aidha, amebainisha kuwa Serikali itatafuta meli ya mizigo itakayofanya safari zake baina ya Unguja na Pemba.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeliagiza Shirika la Meli la Zanzibar kutoiachia sekta binafsi pekee kufanya kazi za usafiri baharini ili kukabiliana na tatizo hilo, na kueleza kuwa meli ya MV Mapinduzi (2) itaanza kufanya kazi hivi karibuni baada ya kufanyiwa matengenezo.
Amesema hatua ya kuimarika kwa bandari za Pemba itachochea sekta binafsi kuleta vyombo zaidi vya usafiri na kusaidia juhudi za Serikali za kumaliza tatizo hilo.
Alhaj. Dkt. Mwinyi amewaasa waumini wa dini ya Kiislamu kuitumia misikiti kwa kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili watu wa makundi maalumu wakiwemo wajane, mayatima na wasio na uwezo.
Amempongeza mfadhili wa msikiti huo, mfanyabiashara Ndg. Said Nassor Bopar, kwa kujitolea kujenga msikiti huo na kuwanasihi watu wenye uwezo kuwekeza katika mambo ya kheri kwa ajili ya Akhera yao.
Kwa mara nyingine, Alhaj. Dkt. Mwinyi amewasisitiza wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa za chakula wakati wa Ramadhan, kwani bidhaa hizo zipo za kutosha, pamoja na kuwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuzidisha ibada na kuhurumiana baina yao.






Comments
Post a Comment