DKT MWINYI: MASHINDANO QURAAN YANAITANGAZA NCHI KIMATAIFA


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi leo, t28 Februari 2026, amehudhuria fainali ya Mashindano ya 22 ya Kimataifa ya Quraan Tajweed yaliyoandaliwa na Taasisi ya Khidmatul Quran Tanzania katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), jijini Dar es Salaam, yakihusisha washiriki kutoka Mataifa 12 Duniani.


Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa mashindano hayo ni jukwaa muhimu la kuimarisha mapenzi ya Quraan, kukuza vipaji vya vijana na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia taaluma ya usomaji wa Quraan. 

Usomaji wa Quraan kwa kuzingatia kanuni za Tajweed si tu taaluma, bali ni msingi wa kujenga kizazi chenye maadili mema, nidhamu ya kiroho na hofu ya Mwenyezi Mungu.

Ameipongeza Taasisi ya Khidmatul Quran kwa kuendeleza mashindano haya kwa kiwango cha kimataifa, jambo linaloipa nchi yetu heshima na hadhi kubwa. Vilevile, amewapongeza washiriki wote kwa ustadi wao wa hali ya juu na kuwashukuru wadhamini, hususan Benki ya CRDB kupitia kitengo cha Al Barakah, kwa mchango wao katika kufanikisha tukio hilo.


"Nimetoa wito kwa wadhamini na waumini wa Dini ya Kiislamu kuunga mkono miradi inayotekelezwa na Taasisi hiyo, ikiwemo ujenzi wa Skuli ya Quraan na Kituo cha masomo ya Dini ya Kiislamu, kwani huu ni uwekezaji muhimu katika malezi ya kizazi chenye misingi imara ya maadili na elimu ya dini" alisema.




Washindi wa mashindano hayo ni Bilal Seif kutoka Misri (97%) aliyepata Dola za Kimarekani 5,000, Muhammad Hussein kutoka Malaysia (90%) aliyepata Dola 3,000, na Hassan Kesi kutoka Tanzania Bara (89.5%) aliyepata Dola za Kimarekani 2,000.


Dkt. Mwinyi aliitimisha kwa kusema Quraan ni mwongozo wa maisha. Tuendelee kuisoma, kuielewa na kuiishi katika matendo yetu ya kila siku.

Comments