CCM YARIDHIA MAZUNGUMZO NA ACT ZANZIBAR
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
HALMASHAURI Kuu ya CCM Taifa katika kikao chake kilichofanyika 19 Februari 2026, Zanzibar chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeridhia kuendelea kwa mazungumzo na ACT Wazalendo ili kupata muafaka wa uundwaji Serikali ya Umoja wa kiTaifa.
Akizungumza Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar mara baada ya kikao hicho, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema mazungumzo hayo yalianza lakini yalikuwa hayajaletwa rasmi kwenye chama.
"Mazungumzo na ACT yalisha anza na upande wa CCM yanaongozwa Rais Wastaafu, Dkt. Ali Mohamed Shein na Dkt. Amani Abeid Karume na sasa chama kimepokea taarifa rasmi ya mazungumzo hayo" alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa ingawa serikali hiyo ipo kikatiba kulingana na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar lakini kwa kuwa katika sura haijakamilika kwa maana ya kujazwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na nne za Mawaziri kulingana na idadi ya kura na asilimia ambazo chama kimepata.
"Kwa kauli moja, kikao cha Halmashauri Kuu CCM Taifa, kimepokea taarifa hiyo na kimeridhia Rais wastaafu, waendelee na mazungumzo na ACT na kukifahamisha chama kila hatua ya mazungumzo" alisema Mwenezi Mbeto.
Alisema kuwa baadae watakapokubaliana wote ACT na CCM suala hilo litawasilishwa Kamati Maalum CCM ambao tutawasilisha Kamati Kuu.
Alisema watatoka na kauli moja katika yale waliyokubaliana hivyo Rais hao wastaafu wataendelea kuwa ndio wasimamizi wakuu wa CCM katika mazungumzo hayo na wasaidizi wao.
Mbeto alisema kupitia mikutano yao ni kwamba ACT walishaliwasilisha kwenye chama chao na likapata ridhaa hivyo nao CCM kimetoa ridhaa mazungumzo yaendelee na agenda zitajadiliwa ili kuzaa muafaka kwa pande zote mbili.
"Wenzetu wameleta ajenda nyingi, kila moja itajadiliwa kwa kina na mwisho wa mazungumzo tutasaini tulichokubaliana na kama ni mfumo wa uchaguzi lazima vyombo vingine vihusishwe" alisema na kuongeza kuwa yale ya kisheria ikiwa ni pamoja na kura ya mapema lazima liende Baraza la Mawaziri na baadae Baraza la Wawakilishi.
Alieleza kuwa yale ambayo yapo kwenye mamlaka ya Rais kutekeleza kupitia mkutano huo, ameshapata baraka za chama.

Comments
Post a Comment