ATHARI ZA KIAFYA WAKATI WA MAJANGA ZAJADILIWA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI inaendelea na mikakati ya KAO kukabili matukio na athari za kiafya zitokanazo na majanga ya dharura na kutathmini kwa kina changamoto za kiafya zinazojitokeza wakati na baada ya majanga, pamoja na kuimarisha mikakati ya maandalizi na uhimilivu wa sekta ya afya wakati wa dharura.
Kupitia kikao kazi kinachofanyika, Dodoma, washiriki wanajadili majanga mbalimbali yanayoathiri afya za wananchi yakiwemo mafuriko, ukame, ajali za barabarani, milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku wakibainisha umuhimu wa mifumo madhubuti ya tahadhari ya mapema na uratibu wa wadau.
Kikao hicho pia kinaweka msisitizo katika kuimarisha huduma za dharura kuanzia ngazi ya jamii, vituo vya afya hadi hospitali za rufaa, ikiwemo kuboresha maandalizi ya rasilimali watu, vifaa tiba na mifumo ya rufaa wakati wa majanga.
Kikao kazi hicho kimeandaliwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na binafsi, kikilenga kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kupunguza athari za kiafya zitokanazo na majanga ya dharura na kulinda ustawi wa afya za wananchi katika mkoa wa Dodoma.



Comments
Post a Comment