WAZIRI KAIRUKI ATAKA UJUMUISHI WANAWAKE, VIJANA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, anasema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kifedha na kitaasisi ili kuchochea uvumbuzi unaojenga ajira na kujitegemea kwa Taifa.
Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la 9 la Mwaka 2026 la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TAIC 2026) 19 Januari 2026, Waziri Kairuki alisema serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijigitali na uvumbuzi wa kiteknolojia.
“Nimefurahi kuona jukwaa hili limetenga siku hii kwa ajili ya wanawake katika TEHAMA kwani wana mchango mkubwa katika kuiendeleza na kuanzisha bunifu na kuongoza taasisi za kijiditali” alisema.
Alibainisha kuwa pia wana nafasi kubwa ya kubuni suluhisho zenye athari chanya za kijamii na kusisitiza umuhimu wa vijana katika mabadiliko ya kidijitali akieleza kuwa kupitia kampuni changa za TEHAMA (ICT STARTUP}. Vijana wana fursa kubwa kujiajiri badala ya kuajiriwa.
Ni malengo ya Serikali kuwa na kundi hili tambulika, liendelezwe na liungwe mkono kwenye kuboresha ubunifu wao” alisema Waziri Kairuki na kuongeza kuwa hatua za kimkakati zinazochukuliwa na serikali ni kuhakikisha mabadiliko ya kidijitali yanatekelezwa kwa ufanisi.
Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya TEHAMA, kuimarisha usajili na uendelezaji wa watalaam pamoja na kuiboresha mifumo ya kusimamia na kusaidia Kampuni changa bunifu ili ziweze kuingia sokoni kwa ufanisi.
Alizitaka taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuwasilisha taarifa kuhusu mifumo yao ya TEHAMA kwa wizara na kuhakikisha mifumo hiyo inasomana na mingine.
Pia Waziri Kairuki alisisitiza umuhimu wa wabunifu na waandaaji wa mahudhui (Content Creator), kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya mifumo na teknolojia zinazoibuka ikiwemo ya Akili Unde (A1) ili kuepuka matumizi yanayokiuka maadili nchini.




Comments
Post a Comment