MBETO ; VIJANA MSIPOTOSHWE HISTORIA ZANZIBAR
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
VIJANA wametakiwa wasikubali kupotoshwa na badala yake wasome historia ya nchi yao ili kujijengea uzalendo na kujua imetoka wapi, ilipo na inapoelekea.
Akizungumza Mjini Unguja ikiwa ni sehemù ya kuhitimisha maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema wasipoijua vizuri historia ya nchi yao watatumiwa vibaya na watu ambao kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar walinufaka wao kwa kuwa na huduma zote za kijamii huku walio wengi wakiwa katika umaskini wa kutupwa katika vibanda vya makuti.
Mbeto alisema Mapinduzi yamekuja kuleta huduma bora kwa watu wote na kuondoa matabaka na utawala wa kigeni uliokuwa unasimamiwa na Uingereza.
"Kuna watu wanapotosha kuwa yalikuwa mauaji na waliopinduliwa walishinda kihalali baada ya uchaguzi mkuu wa 1962 hilo si kweli, ZPPP, ASP na ZNP kila chama kikishinda viti vyake huku ASP kikiongoza kwa wingi wa kura" alisema Mwenezi Mbeto.
Alibainisha kuwa baada ya Uingereza kuona kuwa kwa matokeo yale ASP inaenda kukabidhiwa mamlaka ya kutawala Zanzibar wakatangaza utaratibu kuwa ZPPP na ZNP viti na kura zao zitaunganishwa pamoja na kulinganisha na za ASP na ndipo vyama hivyo vikatangazwa washindi tena kwa idadi kubwa ya viti na sio wingi wa kura.

Kwa mantiki hiyo Zanzibar ingekuwa na Waziri Mkuu ambaye lazima athibitishwe na Falme ya Uingereza na angekuwa anawajibika kwa Sultani.
Hali hiyo inatokea wakati wananchi wenyeji wakiwa hawana huduma zozote za msingi na hawavuki kutoka walipotelekezwa mashambani kuja Mjimkongwe na Darajani kwenye huduma zote za msingi ambazo zilikuwa kwa ajili ya Waarabu, Wazungu, Wahindi na jamii ya Goa kutoka India.
Mbeto alisema mZanzibari aliyeonekana kwenye viunga vya mji huo ni Bawabu (walinzi nje ya maduka) au Makuli (wabeba mizigo) Pwani na wenyeji hawakupewa fursa za huduma za afya, elimu, miundombinu ya njia na barabara wala makazi bora.
"Unajua alikuwa anasema mtoto wa nani? Kuna mtoto gani wa mwananchi mwaAfrika masikini aliyesoma Forodhani mathalani..? Hakuna" alisema Mwenezi Mbeto.
Mwenezi alitanabaisha kuwa Dkt. Mwinyi ataondoka 2030 ni vijana wengi watajitokeza kuwania nafasi hiyo hivyo ni lazima wajitambue na kuiga mfano wa vijana wa wakati huo walioleta mapinduzi, uhuru na ukombozi
" Yote hawawezi kuyajua bila kusoma historia na kufanya utafiti kwa kuzungumza na wazee ambao bado wapo hai ili kujua nchi yako ilitoka wapi, ilipo na inapoenda ili kuweza kupita kwenye misingi na azma nzima ya Mapinduzi kama walivyofanya Rais wote waliopita hadi sasa wa awamu ya nane, Dkt. Hussein Ali Mwinyi" alisema Mwenezi Mbeto.
Maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Zanziba safari hii yamefanyika kwa kwa kipindi cha takribani mwezi mzima kwa viongozi wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo shule za ghorofa, viwanja vya kisasa vya soka ukiwemo wa Gombani Pemba, masoko.viwanda, barabara za juu (Flyover), bandari, Ujenzi wa Uwanja wa ndege mkubwa wa kisasa Pemba na Februari mwaka huu yanazinduliwa mabasi ya kwanza ya umeme Zanzibar na Afrika Mashariki na ya Kati kwa ujumla.





Comments
Post a Comment