MBETO: MIUNDOMBINU YA SOKA ZANZIBAR ITUMIKE KUTUNZA HISTORIA

                                        Na Mwandishi Wetu Madrid, Spain

MIUNDOMBINU ya michezo inayojengwa hivi sasa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi hususan soka inaweza kutumika kuhifadhi historia ya mchezo huo, wachezaji wa zama zote wa timu ya Taifa na kufanywa kuwa chanzo cha mapato kwa watu kutembelea kwa kulipa viingilio na sio kusubiria kunapokuwa na mechi pekee.

Akizungumza wakati alipofanya ziara katika Uwanja wa Santiago Bernabue wa klabu ya soka ya Real Madrid nchini Spain, Katibu wa Kamati Maalum NEC, Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema viwanja ni chanzo cha mapato hivyo wizara husika ijiandae kwa ajili ya kuutumia uwanja wa michuano ya AFCON 2027 kuiingizia serikali mapato na hata klabu pia watambue hilo kuwa viwanja ni vitega uchumi na pia ni sehemu ya kuhifadhi historia na jinsi gani miundombinu hiyo inavyoweza kuvutia watu kutembelea.

"Leo tumepata bahati ya kutembelea Santiago Bernabue na kuna foleni ndefu ya watu waliokuja kuutembelea na kila mmoja analipa Euro 45 kuingia" alisema Mbeto.

Alibainisha kuwa watu wanatembezwa na kuelezwa historia ya klabu, picha za wachezaji wote waliopita klabu hiyo na mataji ambayo wamewahi kuchukua.

Pia upande mwingine Mbeto anasema wachezaji wanaosajiliwa kwa mamilioni ya pesa hawaishii tu uwanjani bali pia wanaingizia klabu mapato kwa watu kuchagua mchezaji na kuonyeshwa kila kitu kumhusu na pia kupiga picha nae.

"Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na michezo wajipange ili uwanja huo wa AFCON uweze kuhifadhi historia ya soka la Zanzibar na timu ya Taifa kwa ujumla wake" alisema Mwenezi Mbeto.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA