DKT. MWINYI: ZANZIBAR KUWA KITUO UTALII WA MICHEZO


                                            Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kujenga miundombinu sekta ya michezo ili kuifanya Zanzibar kuwa Kituo Maalum cha Utalii wa Michezo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo 01 Januari 2026 aliposhiriki Bonanza la 16 la Mazoezi ya Viungo lililoandaliwa na taasisi ya Zabesa, ambalo limeshirikisha vikundi vya mazoezi 165 kutoka vilabu 25 vya Pemba, 100 vya Unguja na 40 kutoka Tanzania Bara na kushirikisha zaidi ya watu 500 na kufanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dkt. Mwinyi alisema mazoezi ya viungo ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu kwani huimarisha afya ya mwili na akili pamoja na kuongeza kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

"Bonanza hili la kila mwaka ni jukwaa muhimu la kuwakumbusha wananchi kuwa afya njema ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla" alisema.

Rais Dkt Mwinyi amewahimiza wananchi kuendelea kushiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, Wavu, riadha pamoja na michezo ya asili ya kitamaduni ili kuimarisha afya zao.

Alisema Serikali itaendelea kuhimiza kufanyika kwa mabonanza mengi zaidi, matukio ya michezo, ligi na mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ili kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha utalii wa michezo.

Aidha amesema michezo ni sekta muhimu katika kuchangia maendeleo ya utalii na uchumi wa Taifa, kwani kupitia michezo Zanzibar inaweza kuvutia watalii na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana na pato la Taifa.

Alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo ili kuimarisha miundombinu ya michezo kwa lengo la kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na kuendeleza sekta hiyo.

"Malengo ya Serikali ni kukuza sekta ya michezo na kuibua vipaji kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, pamoja na kuwaandaa vijana kuwa wanamichezo wenye uwezo wa kushindana kimataifa" alisema Dkt Mwinyi.

Alibainisha kuwa kupitia programu madhubuti za mafunzo, nidhamu na usimamizi bora wa michezo, Zanzibar inaweza kutoa wanamichezo bora watakaouza vipaji vyao katika ligi na vilabu mbalimbali na hivyo kuinua hadhi ya Taifa pamoja na kuboresha maisha yao na familia zao" alisema.

Dkt. Mwinyi alitanabaisha kuwa Serikali imeimarisha kwa kiwango kikubwa sekta ya michezo kupitia ujenzi wa miundombinu ya kimataifa ikiwemo Uwanja wa Amaan Complex, Gombani na Mao Tse Tung, sambamba na ujenzi wa viwanja 17 unaoendelea katika mikoa yote nchini na baadhi tayari vimekamilika.

Rais Dkt. Mwinyi pia ametoa maelekezo kwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya viwanja hivyo ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuvitumia ipasavyo.

Alisisitiza kuwa Zanzibar itaendelea kuwa kisiwa cha amani na kuwataka wananchi kuheshimiana, kushirikiana na kutatua changamoto kwa njia ya majadiliano ili kuimarisha umoja na mshikamano, sambamba na kuyadumisha na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar yanayotimiza miaka 62.

Mapema, Rais Dkt. Mwinyi aliwaongoza mamia ya wana mazoezi ya viungo akiwemo mshindi wa medali ya dhahabu ya mbio za Marathon, Alphonce Simbu,

Matembezi yalianzia Michenzani, Muembe Kisonge hadi Uwanja wa New Amaan Complex.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA