DKT. MWINYI MUUMINI WA UCHUMI WA KIDIGITALI


                                              Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Miaka mitano iliyopita, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati anaingia madarakani miongoni mwa vitu vya mwanzo kufanya ni kutekeleza ahadi yake ya mageuzi ya kiuchumi.

Wananchi wake wanasema akitumia akili kubwa bila mabavu, kufoka majukwaani, kusukumana na wakandarasi site au kuvamia ofisi za umma na kutoa vitisho, Dkt. Mwinyi anafanya mageuzi.

Mageuzi ambayo ndani ya miaka mitano iliyopita yamehuisha Pato la Ndani la Taifa (GDP), kutoka asilimia 3 za awali hadi 7.2 kwa mwaka 2025 huku matumizi ya Tehama yakitajwa kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji huo.

Kulingana na taarifa ya hivi karibuni, uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 7.2 kutoka 3 za Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi Zanzibar (sasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, Fedha na Mipango), Dkt. Saada Mkuya, anasema siri ya mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi (SMZ) kiuchumi ni kutokana na ubunifu wa Rais Dkt. Mwinyi.

Anasema Dkt. Mwinyi alipoingia madarakani alizindua mageuzi ya kiuchumi yanayolenga matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidigitali katika ukusanyaji mapato yote ya serikali, udhibiti wa matumizi na kuzuia uvujaji wa mapato.

Dkt. Saada Mkuya anasema Rais Dkt. Mwinyi ilianza kuhakiki na kuratibu madeni ambayo serikali inadaiwa na watu mbalimbali wakiwemo watoa huduma.

Anasema walipitia uhalali wa madeni hayo na kuyaingiza kwenye mfumo yaliyo halali kwa ajili ya malipo na yenye walakini kuyaweka kando na anabainisha kuwa eneo hilo kulikuwa na upotevu mkubwa wa mapato ya serikali.

Dkt. Saada anasema mfumo huo wa kidigiti upo pia kwenye sekta za afya, uwezeshaji na huduma zingine na anabainisha kuwa kupitia mfumo wa kidigiti kumeondoa uchelewaji na urasimu.

“Kabla ya mwaka 2021 kandarasi ya barabara hadi kutolewa na pengine malipo kufanywa kwa mkandarasi kungechukua hadi miaka mitatu lakini sasa ni tofauti” anasema.

Anabainisha kuwa hivi sasa inachukua si zaidi ya wiki mbili makandarasi anakuwa amelipwa kinachostahiki kulingana na mkataba na kimsingi mianya ya upotevu wa mapato imezibwa na udhibiti wa matumizi nao umekuwa wa kiwango cha juu hivyo kufanya serikali kunufaika na makusanyo yake.

Mageuzii hayo katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na matumizi yake, ndani ya miaka mitano iliyopita hadi sasa kumefanya kuwepo udhibiti wa mfumuko wa bei na kuchangia ukuaji wa sekta za utalii, kilimo na uvuvi.

Rais Dkt. Mwinyi akizungumza 20 Oktoba 2025, wakati wa hafla ya kumpongeza na ugawaji wa gawio kwa wanahisa waliowekeza Zanzibar Skuk anasema mageuzi hayo ya kiuchumi anayotekeleza yamekuwa msingi muhimu unaoijenga Zanzibar.

Anasema fedha zilizowekezwa Zanzibar Skuk ndio ambazo yameiwezesha serikali kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati na kutoa gawio la kwanza ndani ya miezi sita kama sheria ya huanzishwaji wake na hali hiyo anasema ni ishara ya uwajibikaji na uadilifu katika kusimamia dhamana za Taifa ambalo linatengeneza mifumo ya kisasa ya uchumi na biashara.

Alisema hatua hiyo inaonyesha mageuzi mapya ya kiuchumi yaliyotekelezwa na serikali yake ya Awamu ya Nane, ambayo yamekuwa msingi muhimu wa kuijenga Zanzibar mpya inayowashirikisha wananchi katika kuijenga nchi.

Anasisitiza kuwa serikali yake itaendelea kutumia mifumo ya kidigitali katika nyanja na sekta zote katika ukusanyaji, udhibiti wa matumizi na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato.

Kupitia mifumo ya kiDigitali, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZARA), ndani ya miaka mitano iliyopita makusanyo yake yamepanda kutoka TShBilioni 20 hadi TShBilioni 80 wakati Mamlaka ya Mapato (TRA) yakiongezeka kutoka TShBilioni 20 hadi TShBilioni 50.

Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar. Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis anakiri ubunifu wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi ulivyoleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kuwezesha miradi isiyofikiriwa kutekelezeka.

“Leo Zanzibar yote na Pemba zinaenda kuunganishwa na mitandao ya ndani ya barabara za kisasa zinazozingatia watumiaji wote wakiwemo waenda kwa miguu” anasema Mwenezi Mbeto.

Miundombinu hiyo ni tofauti na majengo ya ghorofa kwa ajili ya shule za msingi na sekondari Mjini na Vijijini zenye mahitaji yote muhimu  zikiwemo maabara za masomo yote ya sayansi.

Pia shule hizo zina walimu wa kutosha walioboreshewa stahiki zao, vyumba vya kompyuta maktaba za kisasa zinazosimamiwa na Shirika la Maktaba ya Taifa na madarasa zaidi ya 20 yanafanyiwa majaribio ya ufundishaji kwa kutumia Tehama.

Shuke hizo za majaribio zina ubao wa kielektroniki (Smartboard), uliounganishwa katika mfumo wa Internet ambao unamuwezesha mwalimu kufundisha bila kulazimika kuingia darasani au kufundisha somo husika zaidi ya darasa moja kwa wakati mmoja kwa shule tofauti.

Mbeto anasema ukiacha utalii na vyanzo vingine vya mapato, Zanzibar hivi sasa inakopesheka na benki zinaikimbilia kuikopesha kwa kuwa wanajua ina uwezo wa kulipa kupitia vyanzo vyake ukiwemo mfuko wa madeni.

 “Kila mwezi Rais aliagiza katika mapato ya serikali, zitolewe Dola za Marekani Milioni 15 na kuwekwa kwenye akaunti ya madeni fedha ambayo sawa na Dola Milioni 180 kwa mwaka” anasema.

Chanzo kingine anakitaja kuwa ni pesa za mfuko wa barabara ambazo pato lake ni tozo kwenye mafuta kuanzia ya ndege zinazotua Unguja na Pemba kila siku hadi ya boda boda na vipando vingine.

“ Road Toll (fedha za mfuko wa barabara) ni chanzo cha mapato kinachosimamiwa kidigitali na kuwezesha miradi ya ujenzi wa miundombinu kutekelezeka kwa wakati” anasema Mbeto na kuongeza kuwa Dkt. Mwinyi ni 'muumini' wa mfumo wa kidigital katika kila sekta.

Ujio wa mabasi ya umeme, teksi za baharini na miradi mingine mikubwa, Mbeto anasema ni sehemu ya matumizi ya mifumo ya kidigitali kijamii na kiuchumi hivyo kuinua Taifa kimapato na pia kuwezesha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wakati.

Mfumo huo ambao umekuwa na matokeo mazuri katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato ambao unaifanya Zanzibar kuwa ya kipekee na ya namna yake kimaendeleo kulinganisha na kwingineko.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA