DKT MWINYI: MAAGIZO MATATU AKIZINDUA FLYOVER
Na Mwandishi Wetu. Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua barabara ya juu (Flyover), eneo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi 'B', Mkoa wa Mjini Magharibi na kutoa maagizo matatu kwa wananchi ili serikali iweze kutimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inaenda kuinua hali ya maisha ya walio wengi na kukuza uchumi na pato la Taifa.
Akizungumza wakati wa kuzindua barabara hiyo ambayo imegharimu TSh.Bilioni 23.7, Dkt. Mwinyi alisema jambo la awali anawaomba wananchi kuitunza miundombinu ya barabara, madaraja na flyover zinazojengwa kwani hayo ndio maendeleo ya kweli na barabara zinapojengwa katika maeneo wanayoishi thamani ya nyumba na ardhi zao zinaongezeka.
"Leo hapa tukizungumzia nyumba zilizopo pembeni ya barabara hii bei zake sio zile za zamani na si mjini tu bali hata vijijini zilipopita barabara thamani ya ardhi imepanda, nyumba zimepanda ili mradi maendeleo ya kweli husababishwa na miundombinu" alisema.
Rais Dkt. Mwinyi ambaye alikubali iitwe Dkt. Hussein Mwinyi Flyover alisema, kauli mbiu ya CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar 2025 ni 'Uongozi unaoacha alama' hivyo anafurahi kuzindua flyover ya kwanza Zanzibar na kwamba kaulimbiu hiyo inatekelezwa kwa vitendo wananchi wana dhamana ya kuitunza miundombinu illi idumu muda mrefu na kubaki kama lilivyo sasa.
"Sio limeharibiwa, haribiwa, limegongwa taa zimevunjika. Tunataka libaki lilivyo kwa miaka mingi ijayo ili vizazi vijavyo waone alama tuliyoiacha" alisema Rais Dkt. Mwinyi.
Agizo la pili alisema Dkt. Mwinyi kuwa anawaomba wananchi wawe tayari kupisha miradi na serikali itatoa fidia stahiki.
Alisema mtu mmoja asipokubali kuondoka kupisha mradi anakuwa haitendei haki nchi kwani maendeleo yanayofanyika ni kwa manufaa ya umma na si mtu mmoja.
Rais Dkt. Mwinyi aliwatoa hofu wale wenye mashaka ya upatikanaji fidia kuwa serikali haitomdhulumu mtu kila mmoja atapata stahiki zake.
"Mtupe nafasi ya kuleta maendeleo msiwe kikwazo cha maendeleo katika nchi" alisema.
Alibainisha kuwa anajua kuwepo kwa malalamiko kuhusiana na fidia kwa wanaopisha miradi ndio maana hivi karibuni ameunda kamati kufuatilia na kila mmoja atapata haki yake.
Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa jambo la tatu aliisha sema na anarudia kuwataka wananchi kutokujenga kwenye hifadhi ya barabara kwani ni kwa ajili ya huduma zingine za jamii.
"Msijenge kwenye hifadhi ya barabara sababu tunakusudia huduma za maji, umeme, Internet, umeme na njia za waenda kwa miguu hivyo nawaombeni sana nafasi hizi zisijengwe" alisema na kuongeza kuwa njia pekee za kupitisha huduma hizo ni katika hifadhi ya barabara.
"Leo tumejenga barabara kesho maji tunapitisha wapi kwa hata nyaya za umeme zinatakiwa kupita ardhini na sio juu" alisema na kuwataka wananchi kuzingatia maombi na maagizo hayo kwa maendeleo yao na umma kwa ujumla.
Awali Mhandisi Ali Said Bakari alisema Flyover hiyo ina uwezo ea kuhimili hadi tani 70 na imezingatia usalama wa watumiaji ina upana wa mita 40 na njia za waenda kwa miguu.




Comments
Post a Comment