DKT. MWINYI : DHAMIRA YA SERIKALI KUONDOKANA NA SHULE ZA MABANDA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
ZANZIBAR imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga shule za kisasa zenye hadhi, viwango na ubora unaokidhi mahitaji ya elimu ya karne ya 21.
Akizungumza leo 10 Januari wakati wa uzinduzi rasmi wa shule mbili za ghorofa za Ramadhan Haji Faki – Gamba (Unguja) pamoja na Shule ya Ufundi ya Niaba (Pemba), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi alisema, hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali yake ya kuondokana na shule (skuli) za mabanda na kujenga majengo ya kudumu yatakayoongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.
Ameeleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga shule za kisasa zenye hadhi, viwango na ubora unaokidhi mahitaji ya elimu ya karne ya 21.
"Nimewahimiza wanafunzi wetu kusoma kwa bidii na kutumia kikamilifu fursa ya miundombinu bora iliyowekezwa na Serikali, sambamba na ujenzi wa dakhalia (mabweni) yatakayosaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kuishi nje ya mazingira ya skuli (shule)" alisema Rais Dkt. Mwinyi.
Shule ya Gamba imegharimu TSh. Bilioni 11.2 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 800 kwa wakati mmoja.
Shule ya Ufundi ya Pemba ikigharimu Shilingi Bilioni 9.4. Miradi hii imetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA).
"Tunaendelea kuwekeza kwenye elimu kama msingi wa kukuza rasilimali watu na maendeleo endelevu ya Zanzibar" alisema Dkt. Mwinyi.

.jpg)


Comments
Post a Comment