WITO WA AMANI WATAWALA TAMASHA 'IJUKA OMUKA ' KAGERA


 Na Mwandishi  Wetu, Kagera

WITO wa amani umetawala Tamasha la kila mwaka la Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani) ambako Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa, aliwapongeza viongozi wa dini na wananchi kwa kulinda amani ya mkoa wa Kagera.

Fatma Mwassa alisema kama kiongozi wa serikali ataendelea kuwatumikia wanaKagera kwa kusimamia kikamilifu miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa.

Mkuu huyo wa mkoa amewaahidi viongozi wa dini na wakazi wa Kagera kulitangaza na kulifanya tamasha hilo kuwa endelevu litakalowafanya wenyeji waishio ndani na nje ya nchi kuwa sehemu moja na kufanya uwekezaji wa pamoja.

Awali, Shekhe wa Mkoa wa Kagera, akiwakilisha  Baraza Kuu la Waislamu  (BAKWATA), Haruna Kichwabuta alisema, Mkoa wa Kagera umepitia machungu mengi ikiwa ni pamoja na wakati amani ilipotoweka wakati wa uvamizi  wa Nduli Iddi Amin wa Uganda.

"Kagera tumewahi kukumbwa na matukio mengine yaliyopoteza amani, hivyo kupoteza amani kwa mara nyingine ni kukumbushia machungu ya miaka iliyopita" alisema.

Kwa niaba ya makanisa ya Kipentekoste, Askofu Silvester Ayubu alisema kuwa viongozi wa dini wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa stendi kuu ya Bukoba, soko, ujenzi wa chuo kikuu, miradi ya barabara za kimkakati, maji na huduma zingine.

Katika utangulizi wake alisema serikali imefanya jambo kubwa kwa kuleta viongozi ambao wana kiu ya kuleta maendeleo mkoani humo na hivi sasa kuna mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji tofauti na awali.

“Pamoja na kukutana kuomba dua katika tamasha hili, hii ni nafasi pekee ya kushukuru serikali na tunavutiwa na yanayoendelea na tutawaongoza vijana wetu kulinda amani katika mkoa na kujiepusha na vurugu" alisema na kuwataka wazawa kurudi nyumbani kuwekeza.

Abuddushaidi Abbasi, kiongozi wa JOSUTA mkoa wa Kagera, alisema kuwa uwepo wa tamasha hili unawaweka watu pamoja na viongozi wa dini wanatambua juhudi za Mkuu wa Mkoa za kuwaunganisha wananchi pamoja na kuleta matamasha yanayoendelea kuwajenga pamoja na kuwaimarisha.

Alisema katika kipindi hiki ambacho nchi inapitia mambo mengi, ni vyema viongozi wa dini wakapunguza matamko na badala yake wawajenge waumini wao katika mazuri na mwangaza wa kuleta amani na mshikamano.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA