DKT. NCHIMBI KAMPASI YA UDSM BUKOBA IWE KITOVU CHA UVUMBUZI

 


Mwandishi Wetu, Kagera

Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), kimetakiwa kuhakikisha Kampasi Mpya ya Mkoa wa Kagera inakuwa kitovu cha uvumbuzi, ubunifu na mahali ambapo vijana watawezeshwa kuibua mawazo mapya.

Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kampasi hiyo katika kijiji cha Itahwa, wilayani Bukoba leo 15 Desemba 2025, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Nchimbi alisema pia chuo hicho kiwe sehemu ya kufanya ubunifu na kutumia fursa za soko la pamoja la Jumuia ya Afrika Mashariki.

Dkt. Nchimbi alisema UDSM wana wajibu wa kuhakikisha mitaala itakayotumika katika kampasi hiyo inalenga moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya jamii kwa kutoa zaidi elimu-ujuzi (Elimu ya amali) kwa kuwa mkoa wa Kagera na Kanda yote ya Ziwa zina fursa nyingi za kiuchumi.

“Kwa kuwa mkoa wa Kagera unapakana na nchi jirani, uwepo wa kampasi hiyo utatoa fursa na kuvutia vijana katika nchi hizo kuja kujipatia maarifa muhimu” alisema na kuongeza kuwa kampasi hiyo iwe sehemu ya kukuza mtangamano wa nchi za Afrika Mashariki.

Alibainisha kuwa pia ina wajibu wa kuendeleza umajumui wa Afrika ambao umekuwa msukumo wa Chuo Kikuu Dar es Salaam na ana matumaini kuwa kupitia kampasi hiyo UDSM kitatoa mchango mkubwa katika kuendeleza maarifa katika ujasirimali, kukuza ujuzi wa masoko na kuchochea biashara za mpakani.

“Pia kujenga uwezo wa vijana kuhimili ushindani katika soko la kiKanda na Kimataifa na kwamba serikali ya awamu ya sita imejizatiti kuendeleza jitihada za kuleta mabadiliko katika ngazi zote za elimu” alisema Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi.

Aliyataja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi, stadi na maarifa yanayoendana na mahitaji ya soko na kulingana na lengo kuu la Ilani ya CCM 2025-2030 la kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Alisema njia mojawapo ya kufikia azma hiyo ni kuongeza fursa ya elimu kwa vijana katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu bila ada kuanzia shule za msingi hadi sekondari.


Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA