DKT. MWINYI; ZSSF WEKEZENI MIRADI YA UMEME
Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi angependa kuona Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), ikiwekeza kwenye miradi mikubwa zaidi ikiwemo ya umeme.
Alizungumza wakati wa kuzindua nyumba za kisasa za bei nafuu zilizojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), leo 23 Desemba 2025, eneo la Mombasa, Unguja zilizopewa jina la 'Mji wa Rais Hussein Mwinyi'.
Dkt. Mwinyi, alisema kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii inatekeleza miradi mikubwa ulimwenguni.
Alisema ni vema wakajifunze nchi zingine wanafanyaje na akatoa mfano wa Malaysia, Singapore na Indonesia ambako miradi yote mikubwa ya maendeleo inafanywa kwa uwekezaji wa mifuko ya jamii.
"Mfano hivi sasa Zanzibar kuna changamoto kubwa ya umeme hivyo ningependa kuona mkiwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo kama hiyo" alisema.
Alibainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo wa nyumba 76 za makazi na biashara ni mwanzo mzuri kwa ZSSF kuelekea miradi mikubwa zaidi.
"Ukiacha jukumu la msingi la mifuko ya hifadhi ya jamii kutunza maslahi ya watumishi hadi wanaostaafu licha ya kazi kubwa zinazofanywa na mfuko za kujenga masoko, stendi, vituo vya mabasi kwanini msiwekeze kwenye umeme" alihoji Dkt. Mwinyi.
Alisema serikali inaposema inaenda kuacha alama basi iwe kubwa itakayodumu na amehidi kuibadilisha Zanzibar kwa kuwajengea wananchi nyumba bora za kisasa na kuwaondoa kwenye mazingira duni.
Alitaja maeneo ya Michenzani, Kilimani, Kikwajuni, Jang'ombe kote ni maeneo ambako wakazi wake wengi wanaishi katika nyumba duni na ndoto yake ni kuiona Zanzibar mpya yenye mazingira mazuri ya kuishi wananchi.
Alibainisha kuwa walio wengi wanaishi maeneo yasiyopimwa, hakuna barabara wala njia za majimachafu jambo ambalo alisema halikubaliki na Zanzibar inatakiwa iwe na miji mipya ya kisasa yenye mazingira mazuri kwa wananchi.
Nyumba hizo zenye uwezo wa kutosheleza ukubwa wa familia tofauti kila ghorofa lina sehemu ya bustani ya kupumzikia, viwanja vya kuchezea watoto, maegesho ya magari kwa wenyeji na wageni, mfumo wa kuondoa majitaka hadi mtaro mkuu, msikiti na maduka ya biashara.
Mpaka uzinduzi unafanyika, asilimia 87 ya nyumba hizo tayari zimeuzwa.
Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi, Rais Dkt. Mwinyi atazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 17, Zanzibar.

Comments
Post a Comment