DKT. MWINYI: WEKEZENI KATIKA VITU VIKUBWA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza watu wenye maeneo mazuri kufanya vitu vikubwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa badala ya vidogo visivyo na tija ili wao wenyewe na serikali kunufaika na pia kuufanya mji kuwa na mandhari ya kupendeza kama walivyofanya Umoja wa Walemavu Zanzibar.
Wito huo ameutoa 23 Desemba 2025 mara baada ya uzinduzi wa nyumba za kisasa katika 'Mji wa Dkt. Hussein Ali Mwinyi' ambao umeanzishwa, Mombasa, Mkoa wa Mjini, Unguja.
Mradi huo ambao umekamilika ni wa majengo 14 yenye ghorofa 5 yakiwa na nyumba 276 za kisasa, umegharimu TshBilioni 34, chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Wafanyakazi Zanzibar (ZSSF) na kujengwa na Kampuni ya CRJE ya China.
Dkt. Mwinyi alisema wakati wa uzinduzi wa nyumba hizo kuwa anaupongeza umoja huo kwa uamuzi wao wa kukubali eneo hilo kujengwa mradi huo jambo ambalo litawanufaisha wao, serikali na wananchi.
"Eneo hilo wenye ulemavu wangeweza kukataa kwamba hapa tuachieni wenyewe lakini kwa kujua umuhimu wa maendeleo ya Taifa na wao wenyewe watafaidika walikubali" alisema.
Alisema anasisitiza na aliisha lisema na angependa kulirudia kuwa anazindua nyumba hizo, kazi kubwa imefanyika lakini wananchi wengi Zanzibar bado wanakaa katika mazingira duni sana, angependa Zanzibar ibadilike.
"Ningependa kuiona Michenzani mpya, Kikwajuni mpya, Kilimani mpya, Jang'ombe mpya, Kwahani mpya...". alibainisha Rais Dkt. Mwinyi.
Uzinduzi huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar na jumla ya miradi 17 itazinduliwa au kuwekewa jiwe la msingi.

Comments
Post a Comment