DKT. MWINYI: TUTAENDELEA KUJENGA SHULE ZA GHOROFA


 Na Mwandishi Wetu,, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa shule za ghorofa kama suluhisho la kudumu la changamoto ya uhaba wa madarasa na kuondoa hali ya watoto kuingia madarasani kwa zamu, asubuhi na mchana.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali ni kuongeza bajeti ya sekta ya elimu hadi kufikia TSh.Trilioni Moja na kuifanya kuwa sekta mama ya kipaumbele kwa maendeleo ya nchi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 27 Disemba 2025 alipoifungua Shule Mpya ya Msingi ya Kisasa ya Muungano iliyopo Kibanda Maiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amefahamisha kuwa katika utekelezaji wa mkakati huo, tayari Serikali imeshasaini mkataba na Benki ya CRDB wenye thamani ya Tsh. Bilioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa shule 29 za ghorofa, na kwamba maandalizi ya ujenzi huo tayari yameanza katika maeneo ya Fuoni Kibondeni, Jumbi na Chunga kwa Unguja, pamoja na Kiuyu Minungwini, Mchanga Mdogo na Micheweni kwa Pemba kupitia mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

"Mapema 2026 Serikali itaanza ujenzi wa skuli (shule) za ghorofa katika maeneo ya Jang’ombe, Mikunguni, Kianga na Mtoni Kidatu kwa Unguja, pamoja na Kengeja, Wesha na Miti Ulaya kwa Pemba na kwa kutumia fedha za Serikali itajenga nyingine 18 za ghorofa Unguja na Pemba" alisema.

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane tayari imejenga shule 35 za ghorofa, hatua iliyopunguza changamoto ya mlundikano wa wanafunzi madarasani. Hata hivyo, amesema bado yapo maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya mlundikano wa wanafunzi na uendeshaji wa mfumo wa zamu, hususan Mkoa wa Mjini Magharibi ambao una nusu ya wakazi wote wa Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Zanzibar ni visiwa vyenye eneo dogo la ardhi na kwa kuzingatia kasi ya ongezeko la idadi ya watu linalofikia wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka, ni lazima kutumia busara katika matumizi ya ardhi iliyopo.

Ameeleza kuwa uimarishaji wa miundombinu ya elimu si suala la hiari bali ni la lazima ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya mazingira bora ya kujifunzia.

Akizungumzia ujenzi wa Skuli ya Muungano, amesema una maana kubwa katika historia ya misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliolenga kubadili maisha ya wananchi wa Zanzibar kwa kuweka mbele haki, usawa na upatikanaji wa huduma za msingi ikiwemo elimu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kulinda misingi ya Mapinduzi kwa kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa ya elimu bora ili kujenga kizazi chenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuendeleza Taifa lao.

"Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika sekta ya elimu na katika mwaka wa fedha 2025/2026 imepanga kuziunganisha skuli 70 na mkongo wa mawasiliano pamoja na kuzipatia skuli kompyuta za mezani 2,000 kwa ajili ya maabara, kompyuta mpakato 4,000 pamoja na kuanzisha Madarasa Janja 25 (Smart Classroom) kwa lengo la kuongeza ufanisi wa ufundishaji na kujifunzia" alisema.

Rais Dkt. Mwinyi alibainisha  kuwa serikali inatambua kasi ya ujenzi wa skuli mpya na upanuzi wa fursa za elimu unahitaji pia uwekezaji wa kutosha katika rasilimali watu, hususan walimu, na katika mwaka 2024/2025 imeajiri walimu wapya 1,741 ili kukidhi mahitaji ya shule hizo mpya.

Dkt. Mwinyi amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imeendelea na ajira na tayari imeajiri walimu wapya 492, huku lengo likiwa ni kuajiri walimu 1,500 pamoja na kuimarisha maslahi yao.

Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa Skuli ya Muungano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said, amesema shule hiyo yenye ghorofa tatu ina jumla ya madarasa 42, maabara, chumba cha TEHAMA, vyoo 52 pamoja na maktaba.

 Shule hiyo imejengwa na Kampuni ya FUCHS Construction kwa gharama ya Tsh.Bilioni 6.1 na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,890 kwa wakati mmoja kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa kila darasa.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA